Abstract:
Tafsiri hujishughulisha na usafirishaji wa ujumbe ulio katika
maandishi kutoka lugha asilia kwenda lugha pokezi ambao
hufanywa na mwandishi mwenyewe au mtaalamu mwingine.
Makala haya yanachunguza tamthiliya ya Kinjeketile
iliyoandikwa kwa Kiswahili kwa mara ya kwanza mwaka 1969
kisha ikatafsiriwa kwa Kiingereza na mwandishi mwenyewe
Ebrahimu Hussen kama Kinjeketile mwaka huo huo wa 1969.
Kimahususi, makala inachunguza ni kwa namna gani mtafsiri
ameweza kuweka usawa wa ujumbe na mtindo baina ya matini
asilia na matini pokezi wakati yeye ndiye mwandishi wa
tamthiliya hiyo na ameitafsiri mwaka huo huo. Je alitafsiri au
aliandika tamthiliya mpya iliyo katika lugha ya Kiingereza?
Utafiti umetumia mkabala wa kistahilifu linganishi (correlation
qualitative design) kwa kiasi kikubwa japo mkabala wa
takwimu umejitokeza kidogo. Data zimekusanywa kwa
kutumia mbinu ya upekuzi matini (documentary review).
Nadharia ya ulinganifu imetumika katika uchanganuzi wa data
kama ilivyojadiliwa na Nida (1964), Catford (1965) na Newmark
(1988). Utafiti umebaini kuwa tamthiliya ya Kinjeketile ya
Kiingereza ni matini mpya na sio tafsiri kutokana na utofauti
wake katika utangulizi, muundo pamoja na idadi na utumizi wa
majina ya wahusika.