Abstract:
Kila lugha huwa na utaratibu wake wa ukuzaji na uendelezaji wa msamiati. Katika mchakato wa kupata msamiati wa lugha husika, mbinu mbalimbali hutumika. Utohozi ni mbinu mojawapo ambayo lugha huitumia katika kujitajirisha kimsamiati. Ili msamiati uweze kukubalika katika mbinu hii, kuna michakato mbalimbali inayopitiwa. Michakato hiyo huweza kusababisha athari katika lugha pokezi. Utafiti huu umechunguza utohozi wa istilahi za fani ya tiba na kompyuta za Kiingereza katika lugha ya Kiswahili kwa kuangazia michakato na athari zake. Utafiti umefanyika katika jiji la Dar es Salaam hususan katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichoko Wilaya ya Ubungo pamoja na Baraza la Kiswahili la Taifa lililopo Wilaya ya Kinondoni. Nadharia zilizoongoza utafiti huu ni Nadharia ya Fonolojia Zalishi (NFZ) iliyoasisiwa na Noam Chomsky na Morris Halle (1968) pamoja na Nadharia ya Mofolojia Leksika (NML) ambayo mwasisi wake ni Kiparsky (1982). Aidha, data ya utafiti huu ilikusanywa kwa kutumia mbinu za hojaji na uchambuzi wa matini. Data iliyokusanywa ilichambuliwa kwa kutumia mkabala wa maelezo na wa kitakwimu. Matokeo ya utafiti huu yameonesha kuwa lugha ya Kiswahili imetohoa istilahi za fani ya tiba na kompyuta kutoka katika Kiingereza. Pia, utafiti umebaini kuwa wakati wa utohozi wa istilahi katika Kiswahili, michakato mbalimbali ya kifonolojia, kimofolojia na kisintaksia hufanyika. Michakato hufanyika kadiri ya kanuni na taratibu za lugha ya Kiswahili ili istilahi ziweze kukubalika. Michakato ya kifonolojia iliyobainishwa katika utafiti huu ni pamoja na: mchakato wa udondoshaji, uchopekaji, usahilishaji wa irabu unganifu kuwa irabu sahili na mchakato wa ufupishaji wa irabu ndefu. Michakato ya kimofolojia iliyoonekana kutokana na uchambuzi wa data ni pamoja na uambishaji ambao unafungamana na upangaji wa istilahi za Kiingereza katika ngeli za Kiswahili, uchakataji wa istilahi zenye muundo wa maneno ambatani. Kisintaksia, imebainika kuwa istilahi hutoholewa kwa kuhusisha mchakato wa kuchopeka vihusishi kati ya istilahi za Kiingereza. Halikadhalika, utafiti huu umebaini kuwa utohozi wa istilahi za fani ya tiba na kompyuta za Kiingereza katika Kiswahili una athari chanya na hasi katika lugha ya Kiswahili. Athari chanya zilizobainika ni pamoja na zile za kifonolojia, kisemantiki na kileksika. Athari za kifonolojia zilizoonekana katika utafiti huu ni pamoja na muundo mpya wa silabi katika Kiswahili, kuwapo kwa silabi funge katika Kiswahili na athari za kimatamshi zinazoambatana na ufifishaji wa sauti. Athari za kisemantiki zilizobainika ni pamoja na upatikanaji wa dhana za kisayansi pamoja na visawe vilivyotokana na utohozi. Kwa upande wa athari za kileksika, imedhihirika kuwa baadhi ya istilahi za fani ya tiba na kompyuta zimeonekana kuongezeka katika Kiswahili. Athari hasi zilizobainika ni pamoja na zile za kimofolojia kisemantiki na kileksika. Kimofolojia imeonekana kuwa utohozi umesababisha muundo wa istilahi ndefu na zenye kutatanisha katika matamshi. Halikadhalika, matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa kisemantiki kumezuka mfumuko wa visawe katika Kiswahili. Kileksika imebainika kuwa zipo istilahi za tiba na kompyuta zinazotumika mara chache. Utafiti huu unapendekeza kwamba, utohozi wa istilahi za lugha mbalimbali ufuate kanuni na taratibu zinazowekwa katika Kiswahili. Aidha, kuna haja ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili kutumia istilahi za Kiswahili hata kama kuna istilahi mpya zinazotoholewa. Hivyo, mtafiti anapendekeza kuwa pawepo na uhamasishaji wa matumizi ya istilahi za Kiswahili zilizopo ili kuepuka mfumko wa istilahi nyingi zinazorejelea dhana moja. Mtafiti anaona kuwa kuna haja ya kufanya uchunguzi zaidi kuhusu utohozi wa istilahi za Kiingereza katika Kiswahili kwa miaka ijayo kwa kuwa ni bayana kuwa michakato ya utohozi ni endelevu.